Eritrea:maaskofu waomba maelezo kwa serikali ya nchi! - | vatican news

Play all audios:

Maaskofu wa Eritrea wanaomba maelezo kwa serikali kufuatia na tukio la kuwakatalia wawakilishi wa Kanisa la Ethiopia kuweza kuingia nchini Eritrea mara baada ya kutua uwanja wa ndege, katika
fursa ya maadhimisho ya Jubilei ya dhahabu na siku kuu ya mwaka ya Kanisa Kuu la Asmara. NA SR. ANGELA RWEZAULA – VATICAN Kanisa Katoliki nchini Eritrea limeonesha kusononeka kwake dhidi ya
Serikali ya Asmara kufuatia na kutoruhusu kuingia kwa uwakilishi wa kanisa kutoka nchini Ethiopia tarehe 22 Februari 2020. Kardinali Berhaneyesus Demerew Souraphiel, Askofu Mkuu wa Addis
Abeba, Askofu Abune Mussiè Ghebreghiorghis Uqbu, wa Emdeber na Padre Teshome Fiqre Weldetensae, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu nchini Ethiopia walikuwa washiriki katika maadhimisho ya
Jubilei ya dhahabu na sikukuu ya Kanisa la Kidane Mehert, ambayo ni Makao makuu ya Askofu Mkuu wa Asmara, Menghesteab Tesfamariam, lakini walizuiwa katika uwanja wa Mji mkuu wa Eritrea na
kulazimishwa kurudi nchini kwao Ethiopia siku iliyofuata baada ya mjadala mkubwa ambao haukuleta muafaka. WAWAKILISHI WALIKUWA NA VITAMBULISHO HALALI Katika barua iliyoelekezwa kwenye Ofisi
ya mambo ya kidini, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu nchini Eritrea Padre Tesfaghiroghis Kiflom, anaandika kuwa wageni wa ethiopia walikuwa na vitambulisho halali vya kuingia nchini
Eritrea na kupigwa muhuri katika pasport zao kwa muda wa mwezi mmoja na kwa maana hiyo anaomba sababu zilizosababisha waziweze kuruhusiwa kukaa nchini humo. LENGO LA KANISA NCHINI ERITREA
NI KWA AJILI YA HUDUMA NA ZAIDI WENYE KUHITAJI Siku chache zilizopita Askofu Mkuu Ivan Jurkovič, mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya
Kimataifa huko Geneva, katika Kikao cha 43 cha Baraza kwa ajili ya haki za binadamu, alikuwa ametoa hotuba yake kuhusiana na hali halisi ya Kanisa Katoliki nchini Eritrea na kuelezea kwamba
shughuli zake za kihisani, upendo na kijamii ni kwa ajili ya watu wote, kwa kuwa na umakini kwa namna ya pekee wale wenye kuhitaji zaidi bila kubagua na kwamba lengo la kundelezwa ni la
kibinadamu na siyo la kisiasa na ili hatimaye kuweza kuhamasisha haki, amani, mapatano na majadiliano. KUANZISHA MAJADILIANO YENYE TIJA NA HESHIMA Mwakilishi wa kudumu aidha alikuwa
amewatia moyo serikali ya Eritrea ili kuanzisha majadiliano yenye tija na heshima na Vatican kwa mtazamo wa ujenzi wa wakati mwema ujao na matarajio ya amani ambamo haki ya uhuru na kidini
au imani yoyote viweze kuheshimiwa. Vile vile Papa Francisko alipokutana na Taasisi ya Kipapa ya Kiethiopia kunako tarehe 11 Januari 2020, matarajio yake mema yalikuwa ni kwamba Kanisa
Katoliki la Ethiopia na Eritrea liweze kuhakikishiwa uhuru na kuweza kuhudumia kwa ajili ya ustawi wa pamoja wa watu na taifa kwa ujumla.